WALIMU KUSHIRIKI MPANGO WA KUSAIDIA KUFUNDISHA MASOMO YA SAYANSI MASKULINI

Walimu na wanafunzi wa chuo kikuu dar-es-salaam wanashiriki mpango wa kusaidia kufundisha masomo ya sayansi kwa wanafunzi wa skuli mbalimbali sekondari ikiwa ni mpango wa kukabiliana na upungufu wa walimu wa masomo hayo kisiwani pemba.
Akizungumza mara baada ya kuwasili kwa walimu hao huko bandarini mkoani mratib msaidizi idara ya taaluma abrahman mzee juma amesema ujio wa walimu hao ni juhudi za jumuiya ya pemba forever yenye makao makuu yake jijini dar-es-salaam ambayo imejikita katika kutatua changamoto za elimu na afya kwa wananchi wa zanzibar.
Amesema hivi sasa lengo kubwa ni kusaidia wanafunzi katika masomo ya sayansi ili kutatua changamoto iliyopo ya upungufu wa walimu wa masomo hayo maskulini.
Akizungumza katika utambulisho wa walimu hao huko katika ukumbi wa skuli ya sekondari madungu chake chake afisa dhamini wizara ya elimu pemba maalim salim kitwana sururu amewashukuru walimu wanafunzi hao kwa moyo wao wa ujasiri kwa kuamua kwenda kisiwani pemba kwa kutoa msaada wa kielimu ambao utawasaidia wanafunzi kuweza kukabiliana na masomo yao.
Pia amewataka kueka kando utashi wa kisiasa,dini pamoja na masuala ya mapenzi kwa wanafunzi kwani mambo hayo hayataweza kuleta ufanisi na kufikia lengo lililokusudiwa.
Kundi hilo la wanafunzi walimu ambao sita ni wanawake na thelathini na tatu (33) wanaume watakuwepo kisiwani pemba kwa muda wa miezi miwili na nusu.