WANACHAMA WANALAZIMIKA KUFANYA KAZI MUDA WOTE ILI KURAHISISHA KUTATUA KERO ZINAZOWAKABILI WANACHAMA.

Mjumbe wa kamati kuu ya halmashauri kuu ya taifa ya ccm balozi seif ali iddi alisema wanachama wanaochaguliwa katika nyadhifa tofauti ndani ya chama hicho wanalazimika kufanya kazi muda wote ili kurahisisha kutatua kero zinazowakabili wanachama.
Amesema utendaji wao lazima uoane na kazi nzuri inayoendelea kufanywa na chama hicho chini ya usimamizi wa mwenyekiti wa ccm taifa dr. John pombe magufuli.
Balozi seif ali iddi amesema hayo wakati akiufungua mkutano mkuu wa kuwachagua viongozi wa chama cha mapinduzi mkoa kaskazini unguja uliofanyika kwenye ofisi kuu ya mkoa huo iliyopo mahonda mkoa wa kaskazini unguja.
Alieleza kuwa viongozi wanaopaswa kuchaguliwa ndani ya chama katika kipindi hichi cha mabadiliko ya kiutendaji ni wale wenye ubora wa kiutendaji watakaokuwa na uwezo sambamba na uzalendo wa kutumikia sera na ilani ya ccm.
Balozi seif alitahadharisha wazi kwamba wakati wa kuwa na viongozi ndumi lakuwili kwa maana ya sura mbili kwa nyakati tofauti umekwisha na wala haufai tena kutegemea na kasi ya utendaji wa chama ulivyo hivi sasa.
Akizungumzia miradi ya chama balozi seif ambae pia ni makamu wa pili wa rais wa zanzibar aliwakumbusha viongozi waliopewa kijiti cha kusimamia utendaji wa chama hicho kuwa wabunifu wa miradi ya kuendesha chama hicho.
Alisema ubunifu huo kwa kiasi fulani utasaidia kuondokana na dhana ya kuomba omba kwa vile chama chenyewe hivi sasa kina upungufu wa nguvu katika kujitegemea kiutendaji.
Balozi seif alitolea mfano mkoa wa kaskazini unguja umebahatika kuwa na miradi mingi ya uchumi inayoweza kuendesha chama, lakini tatizo liliopo ni usimamizi mzuri wa miradi hiyo.
Mapema katibu wa chama cha mapinduzi mkoa wa kaskazini unguja nd. Mula othman zubeir alisema chaguzi zote zimeshakamilika kuanzia mashina 21, matawi 102, wadi 18 na kumalizia wilaya mbili zilizomo ndani ya mkoa huo.
Nd. Mula aliwapongeza viongozi na wanachama wa mkoa huo kwa kuhakikisha kwamba chaguzi zote zimeendeshwa katika misingi ya amani, haki na taratibu zilizowekwa ndani ya katiba, sera na ilani ya chama cha mapinduzi.
Akimkaribisha mgeni rasmi mwenyekiti wa ccm aliyemaliza muda wake wa mkoa wa kaskazini nguja nd. Haji juma haji aliwashukuru viongozi na wanachama wote wa ccm wa mkoa huo waliomuwezesha kutekeleza majukumu yake katika kipindi chake cha uongozi.
Nd. Haji alisema ushirikiano wa pande hizo ndio ulioleta mafanikio makubwa na kuwataka viongozi wapya kuiga mfano huo kwa nia ya kujenga safu ya ushindi kwenye uchaguzi mkuu ujao wa mwaka 2020.