Wanadiplomasia 136 wa Uturuki waomba hifadhi Ujerumani

 

 

Wizara ya mambo ya ndani ya Ujerumani imesema wanadiplomasia 136 wa Uturuki pamoja na familia zao wameomba hifadhi nchini humu baada ya kushindikana kwa jaribio la Wanajeshi wa Uturuki la kuipindua serikali ya Rais Recep Tayyip Erdogan. Kwa mujibu wa taarifa za vyombo vya habari vya Ujerumani, idadi hiyo imefikiwa kati ya mwezi wa Agosti mwaka uliopita hadi mwezi Januari mwaka huu. Hata hivyo serikali ya Uturuki imeitaka Ujerumani isitoe hifadhi ya kisiasa kwa maafisa wowote wa kijeshi wa Uturuki. Baadhi ya maafisa hao wamewekwa kwenye vituo vya kijeshi vya Jumuiya ya kujihami ya NATO vilivyopo nchini Ujerumani. Ujerumani ndio nchi yenye wanadiplomasia wengi wa Uturuki duniani kutokana na kuwepo na balozi 13 za Uturuki katika miji mbali mbali nchini humu. Takriban raia milioni 1.5 wa Uturuki wanaishi nchini Ujerumani.