WANANCHI KWENDA MAKTABA KUSOMA VITABU NA TAARIFA NYENGINE ZA KUJIFUNZA.

 

Mkurugenzi wa Shirika la Maktaba Zanzibar Sichana Haji amesema kuzinduliwa kwa tovuti ya shirika hilo isiwe sababu kwa wanafunzi na wananchi kutokwenda maktaba kusoma vitabu na taarifa nyengine za kujifunza.

Amesema katika tovuti hiyo haina uwezo wa kuweka vitabu vyote ambavyo vitatosheleza mahitaji ya wananchi na wanafunzi katika kupata fursa ya kujifunza kama unavyokwenda maktaba ambako kutakuwa na vitabu vya aina tofauti.

Mkurugenzi Sichana amesema hayo ukumbi wa mkutano wa shirika la huduma za Maktaba Chake Chake, kwenye kongamano na uzinduzi wa tovuti ya shirika hilo wakati akitowa ufafanuzi juu ya vitabu vitakavyokuwemo katika tovuti.

Amesema baadhi ya vitabu huwezi kuviweka katika tovuti mpaka upate ruhusa za wamiliki wa husika, hivyo bado umuhimu wa kwenda maktaba upo kwani ndio wataweza kupata taarifa tofauti.

Akifanya uzinduzi wa tovuti hiyo ya www.zls.go.tz, Khamis Juma Khamis amesema katika tovuti hiyo wateja kujua vitabu vilivyo na vinapatikana katika shelfu gani, hali ambayo inampa fursa ya kupata huduma bila ya kusubiri mfanyakazi.

Akifunga kongamano hilo Afisa Mdhamini wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Mohamed Nassor amewataka walimu wa skuli kuacha tabia ya kuandaa safari ya kuwapeleka wanafunzi pikniki na baadala yake waandae ziara ya kutembelea maktaba ili wajuwe umuhimu wa huduma hiyo katika suala la kujifunza.