WASICHANA WA CHIBOK WAUNGANA NA FAMILIA ZAO

Wanafunzi wa kike 82 ambao waliachiwa huru hivi karibuni baada ya kushikiliwa na Boko Haram kwa zaidi ya miaka mitatu jana wameungana na familia zao. Wazazi waliokuwa na shauku, walikuwa wakiwatazama watoto wao kuona ni kiasi gani wapiganaji wenye itikadi kali ya Kiislamu walivyobadili maishi ya watoto wao. Wanafamilia waliovalia mavazi nadhifu waliwakumbatia wasichana hao mjini Abuja. Moja ya kundi lilipiga magoti na mwanamke mmoja alinyoosha mikono juu akilisifu kanisa. Wengine walicheza. Wengine waliangua kilio. Wasichana wengi, wengi wao Wakristo, walilazimishwa kuolewa na wenye itikadi kali na kuzaa nao watoto. Wengine wameingia katika itikadi kali na wamekataa kurejea nyumbani. Kuna wasiwasi kwamba baadhi yao wametumika katika kujitoa muhanga.