WATU 315 WAMEBAINIKA KUJIHUSISHA NA MTANDAO WA BIASHARA YA MADAWA YA KULEVYA

 

 

 

 

Jumla ya watu 315 wamebainika kujihusisha na biashara ya madawa ya kulevya preshani inayoendelea ya mapambano ya vita dhidi ya  madawa ya kulevya katika  mkoa wa mjini magharibi ambapo kati ya hao watu 60 wameshakamatwa na 19 wamefunguliwa mashtaka  baada ya kupatikana na hatia.

Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi Mhe Ayuob Mohammed Mahmoud ameeleza hayo katika mkutano maalum  na kamati ya kusimamia ofisi za  viongozi wa kitaifa kutoka Baraza la Wawakilishi waliofika ofini kwake vuga kupata  taarifa ya mapambano ya madawa ya kulevya changamoto na mafanikio yaliyofikiwa  katika utekelezwaji wa tatizo hilo.

Amesema kuwa mikakati ya kudhibiti madawa ya kulevya inakwenda sambamba na vitendo vya udhalilishaji kwa kuibaini mitandao inayohusika na vitendo hivyo na wahusika kuchukuliwa hatua  ili kuhakikisha vitendo hivyo vinatoweka katika Mkoa wa Mjini Magharibi na Zanzibar kwa ujumla.

Mhe Ayoub  ambae pia ni mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama ya Mkoa huo amewahakikishia wajumbe wa kamati hiyo kuwa Serikali ya Mkoa wa Mjini Magharibi  itaendelea na mapambano ya madawa ya kulevya na inaimani kumbwa ya kushinda vita hivyo sambamba na  kuongeza ulinzi  katika maeneo yote yanayotajwa kuhusihwa na vitendo hivyo yakiwemo ya  mipaka ya Bandarini na Uwanja wa Ndege..

Akizungumza katika kikao hicho mwenyekiti wa kamati ya kusimamia ofisi za viongozi wa kitaifa  ya Baraza la wawakilishi Mhe Omar Seif Abeid amesema kuwa vita dhidi ya madawa ya kulevya ni changamoto kubwa inayohitaji mashirikiano ya pamoja kwa wakuu wa mikoa yote na wadau wengine  ili  kunusuru taifa na janga hilo na kufikia malengo

Wakitoa maoni yao wajumbe wa kamati hiyo kwa pamoja wameelezea kuridhishwa na jitihada mbalimbali zinazochukuliwa na serikali ya Mkoa wa Mjini Magharibi kwa kukemea vitendo viovu ambavyo vimekuwa vichangia kwa kiasi kikubwa kuporomoka kwa maadili ya kizanzibari.