WAZAZI NA WALEZI WAMETAKIWA KUONGEZA JUHUDI KATIKA MALEZI YA WATOTO WAO

Wazazi  na walezi  wametakiwa kuongeza juhudi katika malezi ya  watoto wao ili  waweze  kupambana na  vitendo  vya  udhalilishaji  vinavyofanywa  katika  mazingira  wanayoishi.

Akiwahamasisha wazazi na walezi  wa  shehia  ya tomondo kuwaandikisha  watoto  katika ngazi  ya  awali mkurugenzi  wa  idara ya  elimu  msingi  na  maandalizi  bi  Safia Ali  Rijali amewataka wazazi hao kufuatilia nyendo za watoto wao kutokana na kushamiri vitendo  hivyo ili waweze kufikia  azma  ya kuwa wao ni  tegemeo  la  taifa.

Nao  wazazi  waliohudhuria  kikao  hicho  wamesema  wanahofia  kuwaandikisha  mapema skuli  watoto  wao  kwani wanamaliza  masomo  wakiwa  na  umri  mdogo  kunakopelekea  kuwa  na  vijana  wazururaji hivyo wameiomba  serikali  kuandaa  mfumo mzuri wa masomo yatayowasaidia  kujiajiri baada  ya  kumaliza skuli.

Wizara  ya  elimu  na  mafunzo  ya  amali  kupitia divisheni ya madrasa katika idara ya maandalizi msingi imeandaa utaratibu  utakaowawezesha  walimu  wa  skuli  na  madrasa kuwasaidia kusomesha  wanafunzi kwa wepesi  na  ufahamu  zaidi.