WAZIRI WA AFYA ZANZIBAR AMEPOKEA MSAADA WA FILAMU ELFU MOJA MIA SITA ZA X RAY

 

 

Waziri wa Afya Zanzibar Muheshimiwa Hamad Rashid Mohammed amepokea msaada wa filamu elfu moja mia sita  za X ray  kwa ajili ya kuhudumia wagonjwa katika Hospitali za Chake Chake,Wete ,Mkoani na Micheweni.

Akipokea msaada huo huko Hospitali ya Chake Chake Muheshimiwa Hamad amewataka wanyakazi wa Hospitali hizo kuuthamini msaada huo  na kuzitunza vizuri ili  kuweza kutoa huduma kwa wananchi.

Amesema siku zote  kutoa huduma za afya ni kazi  ya ibada  hivyo hawana budi  kufanya   kwa bidii na kuwahudumia wananchi kwa moyo wa huruma huku wakitaraji kupata ujira kutoka kwa Mwenyezi Mungu.

Naye  Naibu Katibu Ofisi ya Mufti Pemba Sheikh Mahmoud Mussa Wadi  akikabidhi msaada huo kwaniaba ya taasisi ya Abdulla Aid  ameipongeza taasisi hio kwa juhudi zake za kushirikiana na  taasisi ya ZOP hadi kuhakikisha  zinapatikana filamu hizo ambazo ni muhimu katika  kufanyia uchunguzi  na  kuhakikisha kwamba mgonjwa anapata tiba sahihi.

Filamu hizo  zitagaiwa kwa mujibu wa mahitaji ya Hospitali husika ikiwa ni pamoja na Chake Chake filamu mia sita, Mkoani mia tano, Wete mia tatu,Vitongoji mia moja  na Micheweni Mia moja.

Hata hivyo taasisi hizo zimeombwa kuendelea kuwa na moyo wa  kujitolea  kwa lengo la kuwasaidia wananchi  ili  kuhakikisha wanapata huduma bora.