WIZARA YA ELIMU KUSHIRIKIANA NA WIZARA YA FEDHA ILI KUHAKIKISHA AZMA YA ELIMU BURE INATEKELEZWA

 

 

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein, ameeleza haja kwa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali kushirikiana vyema na wizara ya Fedha na Mipango ili kuhakikisha azma ya elimu bure inatekelezwa kama ilivyotarajiwa.Hayo aliyasema leo, Ikulu mjini Zanzibar alipokutana na uongozi wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali wakati ilipowasilisha utekelezaji wa Mpango Kazi wa Mwaka 2017/2018, na Mpango Kazi wa Utekelezaji kwa mwaka 2018/2019 ambapo katika mkutano huo Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Idd alihudhuria.Rais Dk. Shein aliueleza uongozi wa Wizara hiyo kuwa ni vyema ukatambua kuwa tayari  wananchi wanamatarajio makubwa na wanaelewa kuwa bajeti ya Wizara ya hiyo imeongezwa na Rais amerudisha elimu bure ya Msingi na Sekondari ambapo wazazi na wazee hawatochangia chochote.Alieleza kuwa ni vyema hatua za makusudi za ufuatiliaji ufuatiliaji wa fedha hizo kwa wakati zikachukuliwa ili kuleta ufanisi na kutekeleza azma hiyo na matarajio hayo ya wananchi.

Dk. Shein alisema kuwa mambo mengi katika Wizara hiyo yametekelezwa vizuri kutokana na usimamizi mzuri wa uongozi uliopo na kutoa pongezi kwa Wizara  hiyo ikiwa ni pamoja na kutekeleza vyema Mpango Kazi wake.Akieleza kuhusu suala zima la ugatuzi Rais Dk. Shein alieleza kuwa ni suala la lazima kutekelezwa na Wizara hiyo na vyema likatekelezwa kwani Serikali imeshaamua  kuwa sekta hiyo iwe ni miongoni mwa Wizara zilizopendekezwa katika zoezi hilo ikiwemo pia, Wizara ya Afya na Kilimo.Aliongeza kuwa katika Wizara zote hizo taasisi zake zote bado zimo hivyo, ni vyema zikashiriki kikamilifu katika ugatuzi kwani kilichopelekwa Mikoani ni madaraka tu na shughuli zote bado ziko Wizarani hivyo ni vyema Wizara ikaongeza kasi ili jambo hilo lifanikiwe.

Pamoja na hayo, Rais Dk. Shein alieleza kuwa skuli binafsi ni lazima zifuate Sheria za nchi ambazo zinafuatwa na Wizara ya Elimu hivyo ni vyema Wizara hiyo kusimamia  Sheria zake na kuhakikishwa zinafuatwa na skuli zote binafsi na itakayokaidi sheria hizo kutafutwe taratibu za kisheria kuziadhibu.Aidha, Rais Dk. Shein alisisitiza kuwa kabla ya kuziadhibu skuli hizo ni vyema wakatumia utaratibu wa kuzielimisha juu ya taratibu hizo na Sheria za nchi ili waweze kuzifuata kwa  ubora na ufanisi mzuri zaidi.Nae Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Idd aliupongeza uongozi wa Wizara hiyo na kusisitiza haja ya kufuatwa kwa Sheria  ili kuepuka ujauzito kwa wanafunzi walioko skuli.

Katibu Mkuu Kiongozi na Katibu wa Baraza la Mapinduzi Dk. Abdulhamid Yahya Mzee aliipongeza kazi nzuri ya uwasilishaji Mpango Kazi huo iliyofanywa na Wizara hiyo huku akisisitiza haja ya kulisimamia suala la ajira kwa skuli binafsi sambamba na suala zima la kufanya tathmini na ukaguzi kwa skuli na walimu wake.Mapema Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Riziki Pembe Juma alieleza kuwa katika mwaka wa fedha  wa 2017/2018, Wizara inaendelea na malengo  ya kupanua upatikanaji wa huduma za elimu na kuimarisha ubora wa elimu inayotolewa.Alieleza kuwa katika kufanya hivyo Wizara imeweka vipaumbele katika kufikia dhamira ya utoaji wa elimu bora kwa wote ambapo Wizara imepanga kujenga Skuli ya Maandalizi ya Mbuyu Maji, kuimarisha vituo vya tutu na kuihamasisha jamii kujenga vituo hivyo vipya katika Wilaya za Magharibi A na B kwa Unguja na Chake Chake kwa Pemba.

Waziri Pembe  alieleza kuwa  Wizara hiyo pia, imeweza kuimarisha Elimu ya Msingi ikiwa ni pamoja na kujenga skuli za msingi ya Kwarara na Pangawe, kukamilisha madarasa 200 yaliyoanzishwa na wananchi yakiwemo 120 Unguja na 80 Pemba, kutoa mafunzo kwa walimu pamoja na kuendelea  utoaji wa huduma ya chakula kwa wanafunzi.Aidha,  alieleza kuwa  utekelezaji mwengine ni kuimarisha elimu ya Sekondari ikiwa ni pamoja na kuendelea na ujenzi wa skuli ya Bwefum na Kibuteni Unguja,kujenga jengo jipya la ghorofa katika skuli ya Biashara Mombasa, kuanza ukarabati mkubwa wa skuli ya Sekondari ya Lumumba na kujenga skuli tisa za ghorofa zikiwemo tano Unguja na nne Pemba.

Aliongeza kuwa utekelezaji mwengine ni  kuimarisha elimu Mbadala na Mafunzo ya Amali ikiwa ni pamoja na kuendeleza ujenzi wa vituo vya Mafunzo ya Amali Makunduchi kwa Unguja na Daya Mtambwe kwa Pemba pamoja na kuimarisha elimu ya juu kwa kujenga maabara ya kusomeshea, kuwapatia mikopo wanafunzi wenye sifa ya kujiunga na elimu ya juu, kutoa ufadhili na kufanya tathmini na ufuatiliaji kwa taasisi za elimu ya juu.Pia, Waziri huyo alieleza kuwa ujenzi wa skuli ya Kwarara kati ya Wakorea na Mkandarasi tayari umeshatiwa saini na matayarisho ya ujenzi huo yameanza pamoja na kuendelea kwa ujenzi wa skuli ya Fuoni Pangawe ambao ujenzi wake umefikia asilimia 50.Alieleza kuwa jumla ya walimu 1,006 waliohitimu Shahada na Stashahada katika masomo ya Sayansi, Hisabati, Jiografia, Historia na Kiingereza wameajiriwa kwa Unguja na Pemba ambapo pia, skuli 100 zimepatiwa vifaa vya michezo na walimu 300 wa michezo wamepatiwa mafunzo kupitia mpango wa Sport 55.

Alisema kuwa mbali na mafanikio yanayoendelea kupatikana katika sekta hiyo ya elimu pia, kuna baadhi ya changamoto zinazojitokeza ikiwemo kasi kubwa ya ongezeko la wanafunzi wanaoandikishwa katika skuli za msingi na sekondari hasa skuli za Mkoa wa Mjini Magharibi .Nao viongozi wa Wizara hiyo walimpongeza Rais Dk. Shein kwa maelekezo yake anayoyatoa kwao hatua ambayo inawarahisishia kutenda kazi zao huku wakimuhakikishia kuwa wanaendelea kutekeleza vyema kazi zao ili kuweza kutoa huduma bora kwa wananchi wote wa Zanzibar.Wakati huo huo, Rais Dk. Shein alikutana na uongozi wa Wizara ya Habari, Utalii na Mambo ya Kale chini ya Waziri wa Wizara hiyo Mahmoud Thabit Kombo ambaye alieleza kuwa  Wizara hiyo ina dhamana ya kusimamia sekta kuu tatu ambazo ni habari, Utalii na Mambo ya Kale.Alieleza kuwa katika sekta ya Habari kuna mafanikio makubwa yaliofikiwa katika utekelezaji wa malengo ambayo yamesaidia kukuza sekta hiyo hapa nchini  ambapo pia, pamoja na fanikio hayo pia, kuna changamoto zinazoikabili sekta hiyo ambazo zinahitaji kufanyiwa kazi ili malengo yaweze kufikiwa katika utekelezaji wake.Aidha, kwa upande wa sekta ya utalii, Waziri Kombo alieleza kuwa sekta hiyo imefanikiwa kwa kiasi kikubwa katika katika kutekeleza malengo yake ambayo yamepelekea kuongezeka kwa idadi ya watalii wanaokuja kuitembelea Zanzibar ambao hutoa ajira kwa wananchi pamoja na kuchangia pato la Taifa.