ZANZIBAR IMEDHAMIRIA KUZIPANDISHA HADHI HOSPITALI ZA SERIKALI

 

Rais wa zanzibar na mwenyekiti wa baraza la mapinduzi dk. Ali mohamed shein amesema serikali ya mapinduzi ya zanzibar imedhamiria kuzipandisha hadhi hospitali za serikali za kivunge na makunduchi kuwa za mkoa katika kipindi kifupi kijacho.

Dk. Shein aliyasema hayo katika chakula cha usiku kilichoandaliwa na wizara ya afya kwa ajili ya kuchangia fedha za kusaidia hospitali ya makunduchi na hospitali ya kivunge ikiwa ni pamoja na maadhimisho ya miaka kumi ya mradi wa kuendeleza huduma za afya zanzibar (hipz).

Katika hotuba yake, dk. Shein alisema kuwa juhudi za mradi wa kuendeleza huduma za afya zanzibar (hipz), sio tu umeweza kusaidia kuziweka hospitali za makunduchi na kivunge katika hali nzuri na bora katika utoaji wa huduma lakini amesema mradi huo umesaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza msongamano wa wagonjwa katika hospitali kuu ya mnazi mmoja.

Dk. Shein alitumia fursa hiyo kutoa shukurani kwa uongozi wa mradi huo wa hipz kwa kuweza kuimarisha huduma za afya, miundombinu, usimamizi na uwajibikaji katika hospitali hizo.