ZANZIBAR INAPASWA KUWA KATIKA ULINZI MUDA WOTE KULINGANA NA MAZINGIRA YAKE

Makamu wa pili wa rais wa zanzibar balozi seif ali iddi amesema lazima tanzania iendelee kubakia salama ili kuwapa fursa wananchi na wageni wanaoingia nchini wafanye mambo yao ya kawaida bila ya usumbufu.
Balozi seif amesema hayo alipokuwa akizungumza na kamanda wa brigedia nyuki zanzibar brigedia general fadhil nondo aliyefika ofisini kwake kujitambulisha baada ya kuteuliwa kushika wadhifa huo hivi karibuni.
Brigedia general fadhil nondo alikuwa akikaimu nafasi hiyo tokea mwezi januari mwaka huu wa 2017 baada ya aliyekuwa akishikilia wadhifa huo brigedia general cyrill ivor mhaiki kufariki dunia mapema mwaka huu.
Balozi seif alisema zanzibar inapaswa kuwa katika ulinzi wa uhakika muda wote kulingana na mazingira yake yaliyozunguukwa na bahari ambayo wakati kwengine hutoa nafasi kwa wahalifu kufanya vitendo vinavyosababisha hofu na shaka kwa wananchi.
Makamu wa pili wa rais wa zanzibar alimuhakikishia brigedia kamanda huyo wa nyuki kwamba serikali ya mapinduzi ya zanzibar na viongozi wake itakuwa tayari wakati wote kumpa ushirikiano wa karibu zaidi ili kuhakikisha anatekeleza vyema dhamana aliyokabidhiwa na taifa.
Hata hivyo katika utekelezaji wa majukumu yake balozi seif alimshauri brigedia general fadhil nondo kushirikiana na makamanda na walinzi wa vikosi vyengine vilivyopo zanzibar ili kazi yao ya ulinzi iende vyema bila ya kukaribisha vikwazo, mikwaruzo au migongano yoyote ile isiyokuwa na faida.
Balozi seif alimtakia kheir na mafanikio katika uwajibikaji wake huo mpya kiongozi huyo mkuu wa jeshi la wananchi wa tanzania { jwtz} kwa upande wa visiwa vya zanzibar.
Mapema brigedia general fadhil nondo alimuahidi makamu wa pili wa rais wa zanzibar kwamba atakuwa tayari kupokea maagizo yoyote atakayopewa kuyatekeleza katika nafasi yake hiyo mpya ya uongozi.
Kamanda nondo alisema kwa mujibu wa mfumo na taratibu za jeshi la wananchi wa tanzania nafasi yake ya kazi inawajibika kutekelezwa kwa kupokea maagizo na ushauri kutoka kwa viongozi wa juu wa eneo analofanyia kazi.
Brigedia general fadhil nondo kabla ya uteuzi huo alikuwa afisa mafunzo na operesheni wa brigedia nyuki pamoja na mkuu wa kambi la jwtz iliyopo bavuai wilaya ya magharibi “b” mkoa wa mjini magharibi zanzibar.