ZANZIBAR ITAKUTANA NA MABINGWA WATETEZI

Zanzibar itakutana na mabingwa watetezi, uganda katika mchezo wa Nusu Fainali ya Kombe la Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati, CECAFA Challenge inayoendelea nchini Kenya, Desemba 15, mwaka huu.
Hiyo itakuwa Nusu Fainali ya pili, baada ya Nusu Fainali ya kwanza kati ya wenyeji, Kenya dhidi ya Burundi Desemba 14.
Na hiyo ni baada ya Kenya kuifunga 1-0 Tanzania Bara katika mchezo wa mwisho wa Kundi A jioni ya leo Uwanja wa Jomo Kenyatta, Kenya.
Kilimanjaro Stars ya kocha Ammy Ninje ilifunguka na kuanza kupeleka mashambulizi langoni mwa Harambee kusaka bao la kusawazisha, lakini hawakufanikiwa. Kenya wanafikisha pointi nane na kumaliza juu ya kundi wakifuatiwa na Zanzibar waliomaliza na pointi saba.
Mechi nyingine ya Kundi A iliyotangulia mchana wa leo, Libya ilishinda 1-0 dhidi ya Zanzibar, bao pekee la Alharaish Zakaria dakika ya 24 Uwanja wa Jomo Kenyatta mjini Machakos, Kenya leo, wakati mchezo wa mwisho wa Kundi B, Burundi iligawana pointi na Sudan Kusini baada ya sare ya 0-0 Uwanja wa Bukhungu mjini Kakamega.
Hiyo inamaanisha Uganda inamaliza kileleni mwa Kundi B kwa pointi zake tano sawa na washindi wa pili, Burundi ambao wanazidiwa wastani wa mabao.