Daily Archives: September 4, 2019

WIZARA NA TAASISI ZA SMZ ZATAKIWA KUSHIRIKIANA ILI KUFANIKISHA UTEKELEZAJI WA MIRADI MBALI MBALI

Rais wa Zanzibar na mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein amesema kuna umuhimu kwa wizara na taasisi za serikali kushirikiana ili kufanikisha utekelezaji wa miradi mbali mbali ya maendeleo kwa wakati.

Dk. Shein amesema hayo Ikulu mjini hapa, wakati akipokea taarifa za Utekelezaji wa Mpango Kazi kwa Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji kwa mwaka 2018/2019.

Alisema kuna baadhi ya miradi ya maendeleo ambayo imeshindwa kutekelezwa kwa wakati, kutokana na ukosefu mashirikiano, baada ya taasisi kuwa na mitizamo inayokinzana  katika suala la uwekaji wa miundombinu.

Alieleza kuwa kabla ya mradi wowote wa maendeleo kuanza kutekelezwa, ni muhimu kwa taasisi zenye miundombinu inayoingiliana kukaaa pamoja na kuangalia namna  miundombinu hiyo itakavyowekwa, ili kuepuka gharama na uharibifu usio wa lazima.

Alisema kuna baadhi ya barabara zilizokatwa kwa ajili ya kupitisha miundombinu bila ya wenye mamlaka kuarifiwa, hivyo alisisitiza umuhimu wa kuendeleza ustaarabu wa kufanyakazi kwa pamoja ili kuzipatia ufumbuzi changamoto zinazojitokeza.

Dk. Shein alitowa ufafanuzi huo baada ya Uongozi wa Wizara hiyo kuelezea changamoto kubwa ya uharibifu wa barabara unaotokana na baadhi ya taasisi kupitisha miundombinu, ikiwemo ya maji na taa.

Aidha, Dk. Shein alisema serikali itaangalia uwezekano  wa kuijenga barabara ya Chake-Wete kwa nguvu za serikali, kwa kuzingatia tayari imejenga uwezo wa kiutendaji baada ya kununua vifaa mbali mbali vya ujenzi wa barabara.

Alisema hayo baada ya taarifa ya tathmin za awali zilizotolewa na Uongozi wa Wizara hiyo kuonyesha gharama kubwa za ujenzi na malipo ya fidia ya barabara hiyo kupitia mkandarasi.

Aliwataka mafundi na Mainjinia wa Wizara hiyo kuwa na uataratibu wa kukaa pamoja na kufanya tathmin ya gharama za ujenzi, kabla ya mradi wowote kuanza kutekelezwa, ili kuepuka na viwango vikubwa vya gharama vinavyotozwa na wakandarasi.

Aidha aliwataka viongozi wa Wizara hiyo kukutana na Viongozi wenzao (Wizara ya Mawasiliano) Tanzania Bara ili kuona mifumo ya kiusalama katika Viwanja vya ndege inafanyakazi kwa maslahi ya pande mbili za Muungano.

Dk. Shein alikumbusha umuhimu wa Bodi za taasisi na mashirika ya Serikali kutekeleza majukumu yao na kufanya maamuzi kisheria, huku akisisitiza haja ya taarifa zao kuwasilisha kwa Waziri anaehusika.

Katika hatua nyengine, Dk. Shein aliutaka Uongozi wa Wizara hiuyo kuzingatia umuhimu wa matumizi sahihi ya mchanga kwa ajili ya miradi yake ya ujenzi wa barabara, kwa msingi kuwa rasilimali hiyo iliyobaki ni kidogo.

Alisisitiza uamuzi wa Serikali wa kutokuagiza rasilimali hiyo nje ya nchi, kwa vile hatua hiyo haina maslahi na Taifa.

Alisema Serikali itaendelea na udhibiti wa rasilimali zake, ikiwemo mchanga, kifusi na mawe, ili kuhakikisha kunakuwepo matumizi mazuri,  baada ya siku za hivi karibuni kubainika baadhi ya watu wakisaga vifusi kwa ajili ya matofali.

Alisema hivi sasa kumebaki maeneo sita pekee yenye mchanga katika ardhi ya kilimo, hivyo kuna hatari ya kuathiri upatikanaji wa chakula, endapo rasilimali hiyo itatumika kwa shughuli za ujenzi.

Aidha, akawataka viongozi wa Wizara hiyo kukaa pamoja na wadau wa usalama barabarani, ikiwemo Polisi, UUB na Manispaa kwa ajili ya kuangalia mahitaji ya uwekaji wa taa za kuongoza gari barabarani.

Alisema katika maeneo mbali mbali ya miji yenye makutano ya barabara  Unguja na Pemba, kunahitajika kuwekwa taa za kuongoza magari pamoja na njia ya wenda kwa miguu (zebra cross), ili kupunguza uwezekano wa kutokea ajali za mara kwa mra, ikizingatiwa baadhi ya madereva na waendao kwa miguu hawafahamu sheria za usalama barabarani.

Alisema miji imekuwa na gari zimeongezeka, hivyo ni lazima kuwepo taa za kuongoza gari katika maeneo yanayoonekana hatarishi ili kuepuka ajali, sambamba na kutaka kuwepo matumizi mazuri ya barabara kuanzia hatua za upatikanaji wa leseni.

Aidha, Dk. Shein aliukumbusha uongozi huo kuwa Serikali imetumia gharama kubwa kufanikisha uwekaji wa Mkonga wa Taifa, hivyo akasisitiza matumizi yake kuwa ni ya umma.

Akinasibisha na kauli yake, alizitaka taasisi zote za Serikali zenye kutoa huduma nchini kukaa pamoja na taasisi nyingine na kutafuta ufumbuzi pale zinapojitokeza changamoto, ikiwemo madeni, badala ya taasisi moja kuikatia huduma taasisi nyingine.

Vile vile, Dk. Shein alisema ili Wizara iweze kupata maendeleo endelevu ni jukumu la kila Idara na taasisi za Serikali kufanya utafiti utakaoleta matokeo ya haraka na kuondokana na dhana kuwa Idara ya Mipango, Sera na Utafiti ndio pekee yenye jukumu hilo.

Alisema hii ni mara ya kwanza katika hsitoria ya Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji kupata fedha zaidi ya shilingi Bilioni 131.6 , akibainisha hatua hiyo inatokana na dhamira ya Serikali ya kuimarisha Wizara hiyo yenye umuhimu mkubwa kwa maendeleo ya Taifa,

Alitowa pongezi kwa Uongozi wa Wizara hiyo na kubainisha kuridhishwa kwake kutokana na utekelezaji wa majukumu, sambamba na uwasilishaji mzuri wa taarifa ya Utekelezaji wa Mpango kazi.

Mapema, Waziri wa Wizara hiyo, Dk. Sira Ubwa Mamboya alisema katika kipindi hicho Wizara imepata mafanikio makubwa, ikiwemo  kukamilisha ujenzi wa kilomita 28 za barabara mbali mbali Unguja na Pemba kwa kiwango cha lami, ikihusisha kilomita 16 za barabara ya Ole – Kengeja, kilomita tatu za barabara ya Wawi – Mabaoni na kilomita tatu za barabara ya Mkanyageni – Kangani.

Alisema Wizara hiyo imefanikiwa kuweka Taa za kuongezea magari katika maeneo ya matano ya makutano ya barabara  Unguja na Pemba, ambayo ni kwa Biziredi, Mlandege na Mtoni Jeshini (kwa Unguja) pamoja na Mtemani Wete na Chake chake PBZ kisiwani Pemba.

Aliongeza kuwa katika kipindi hicho  Wizara imezifanyia matengenezo  barabara mbali mbali kwa kuziwekea kifusi, kuziba mashimo pamoja na kuzifanyia usafi.

Aidha, alisema Wizara inaendelea na ujenzi wa Barabara ya Bububu – Mahonda – Mkokotoni  yenye urefu  wa kilomita 31, wakati ambapo kilomita 28.8 za barabara hiyo zikiwa tayari zimewekewa kifusi tabaka la mwisho, pamoja na kuweka lami ya maji kilomita 14 katika upande mmoja wa barabara.

Dk. Sira  alisema katika kipindi hicho Wizara imekamilisha ujenzi wa mtaro wenye urefu wa kilomita 1.5 katika barabara ya Kiembesamaki, huku ikiendelea kumalizia hatua za mwisho za ujenzi wa daraja katika eneo la Kibonde Mzungu, mradi unaohusisha uwekaji taa, ujenzi wa kingo za pembeni (guardrail) pamoja na uwekaji wa lami ya mwisho.

Akigusia azma ya Serikali katika kuimarisha ujenzi wa miundo mbinu, Dk. Sira alisema Wizara imefanikiwa kununua vifaa mbali mbali vya ujenzi, ikiwemo vifaa 17 vya zana nzito, mitambo ya Lami, gari la kutandazia lami pamoja na gari la lami ya maji ambavyo tayari vimewasili nchini.

Alibainisha kuwa aina 13 ya vifaa vilivyosalia viko njiani kuja nchini.

Aidha, alisema Wizara imefanikiwa kukamilisha ujenzi wa Meli mpya ya Mafuta (MT Ukombozi 11), ambayo tayari imewasili nchini tangu Agosti 7, mwaka huu.

Dk. Sira alisema Wizara kupitia Mamlaka ya Viwanja vya Ndege  imefanikiwa kuimarisha huduma katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume (AAKIA) kwa kuimarisha Ulinzi na usalama , ufungaji wa mkanda wa mizigo, ununuzi wa mashine tano mpya za ukaguzi, kuimarisha Ukumbi wa Marais pamoja na kuendelea na ufungaji wa Vipoza hewa.

Alisema kwa upande wa Pemba, Wizara imefanikiwa kukamilisha upembuzi yakinifu wa Uwanja wa Ndege Pemba, unaoonyesha namna uwanja huo utakavyokuwa baada ya ujenzi na kubainisha kuwa hatua inayoendelea hivi sasa ni ya utafutaji wa fedha ili ujenzi huo uweze kuanza.

Katika hatua nyengine Waziri huyo alisema Wizara imefanikiwa kununua vifaa mbali mbali vya kufanyia kazi Bandarini, ili kuongeza ufanisi katika uhudumiaji wa mizigo.

Alivitaja vifaa hivyo kuwa ni pamoja na vile vya kubebeba mizigo (Reachestaker moja, Mobile crean kubwa ya tani 55 pamoja an Folklift moja, Boti ya Rubani moja na Tishali la kuhudumia vyombo vya abiria katika Bandari ya Malindi.

Alibainisha kuwa malipo ya awali kwa ajili ya ununuzi wa vifaa hivyo tayari umefanyika na kazi ya matengenezo ya vifaa vilivyopo inaendelea.

Nae, Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji Mustafa Aboud Jumbe, alisema changamoto kubwa inayoikabili Wizara hiyo ni baadhi ya taasisi kukata barabara kwa ajili ya kupitisha hduma za kijamii, hivyo kuleta uharibifu mkubwaa wa barabara hizo.

Alisema kumekuwepo ukataji ovyo wa barabara kwa ajili ya kupitisha huduma za maji pamoja na umeme unaofanywa na taasisi bila kuzingatia gharama za utengenezaji wa barabara hizo.

“Kuna baadhi ya wakati taasisi mbili kwa nyakati tofauti hukata barabara kila mmoja na kupitisha miundombinu, jambo ambalo kama kungekuwepo ushirikiano kwa taasisi kukaa pamoja kabla ya ujenzi na kupitisha miundombinu yao katika eneo moja, kusingekuwa na uharibifu huu wa barabara”, alisema.

Wakati huo huo; Rais Dkt Shein alikutana na Uongozi wa Wizara ya Nchi (OR) na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi na kusisitiza haja ya Idara na taasisi za Wizara hiyo kufanya utafiti ili kupata mafanikio katika malengo yake.

Alisema ni muhimu kwa viongozi wa Idara kufanya tafiti mbali mbali, akibainisha hatua hiyo itawezesha kupata maendeleo endelevu.

Aidha, Dk. Shein aliutaka uongozi wa Wizara hiyo kujenga mashirikiano na wafanyakazi wake, ili kuweza kuzipatia ufumbuzi changamoto mbali mbali zinazokwamisha utendaji bora wa kazi.

Dk. Shein aliipongeza uongozi wa Wizara hiyo kwa utekelezaji mzuri wa majukumu yake, pamoja na kuwasilisha vyema taarifa za utekelezaji wa mpango kazi kwa mwaka 2018/2019.

Nae, akiwasilisha taarifa ya mpango kazi kwa Wizara ya Nchi Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Waziri wa Wizara hiyo Issa Haji Ussi ‘Gavu’ alisema katika kipindi hicho Ofisi ya Rais iliendelea na ujenzi wa Ikulu ndogo Micheweni, ambapo hivi sasa imefikia hatua ya kuridhisha .

Alieleza kuwa  ujenzi wa jengo jipya la Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Chake chake Pemba  unaendelea vizuri,  ukitarajiwa kukamilika katika mwaka wa fedha wa 2019/2020.

Aidha,  alisema  Serikali imekuwa na mahusiano mema na Wazanzibari wanaoishi nje ya nchi kupitia Makongamano ya kila mwaka.

OGEZEKO LA WATALII LA ASILIMIA 20.1 LIMECHANGIA KUKUA KWA UCHUMI WA ZANZIBAR

WIZARA ya Fedha na Mipango imeeleza kuwa kuongezeka kwa idadi ya watalii walioingia nchini na kufikia watalii 520,809 mwaka 2018 kutoka watalii 433,474 mwaka 2017 sawa na ogezeko la asilimia 20.1 kumechangia kuongezeka kwa pato la Taifa na kukua kwa uchumi wa Zanzibar.

Waziri wa Fedha na Mipango Balozi Mohamed Ramia Abdiwawa aliyasema hayo leo, Ikulu mjini Zanzibar wakati wizara hiyo ilipowasilisha Taarifa ya Utekelezaji wa Bajeti  pamoja na Mpango wa Utekelezaji wa Bajeti kwa mwaka 2019/2020.

alieleza kuwa kwa mwaka 2018 uchumi wa Zanzibar umeendelea kuwa imara kwa kuongezeka kwa Pato halisi la Taifa pamoja na kushuka kwa kasi ya mfumko wa bei za bidhaa na huduma nchini na kufikia wastani wa asilimia 3.9 mwaka 2018 ikilinganishwa na wastani wa asilimia 5.6 mwaka 2017.

Alisema kuwa kuimarika kwa Pato la Taifa na ukuaji wa uchumi pia, kumechangiwa na kuendelea kuwa tulivu kwa thamani ya Shilingi ya Tanzania dhidi ya Dola ya Kimarekani kwa asilimia 1.6.

Aliongeza kuwa kushuka kwa kasi ya mfumko wa bei za bidhaa na huduma nchini na kufikia wastani wa asilimia 3.9mwaka 2018 ikilinganishwa na wastani wa asilimia umepelekea kuongezeka kwa Pato la Mwananchi kutoka TZS 2,104,000 sawa na dola za Kimarekani 944 na kufikia TZS 2,323,000 sawa na Dola za Kimarekani 1,026.

Alisema kuwa wakati Serikali ikiendelea kutekeleza Dira ya Maendeleo ya Zanzibar ya 2020, Wizara kupitia Tume ya Mipango imeanza matayarisho ya Dira mpya itakayotoa mwelekeo kwa kipindi kirefu kijacho kuanzia mwaka 2021 hadi 2050.

Alieleza kuwa mwelekeo mpya na vipaumbele vya uchumi wa Zanzibar wa uwezekano wa kuwepo kwa mafuta na gesi, mabadiliko ya sera na mipango ya kimataifa, mageuzi ya sayansi na teknolojia na mabadiliko ya tabianchi yanahitaji sera na mikakati mipya ya kutekeleza.

Alieleza kuwa ujenzi wa uwanja wa ndege wa Abeid Amani Karume ni lazima ukatekelezwa ambapo tayari Serikali imejipangia pamoja na miradi mengine ukiwemo ujenzi wa Bandari ya Mpigaduri.

Alisema kuwa viashria vyote vinaonesha kwamba uchumi wa Zanzibar ni imara na unakuwa kwa kasi kubwa sana kutokana na viashiria vilivyopo.

Nae Rais Dk. Shein kwa upande wake aliupongeza uongozi wa Wizara hiyo pamoja na watendaji wake wote kwa kuwasilisha vyema Mpango Kazi na kuutaka kuongeza kasi na kufanya kazi kwa bidii ili mafanikio zaidi yaendelee kupatikana.

Rais Dk. Shein alieleza kuwa zoezi hilo la mikutano ya utekelezaji wa mpango kazi linasaidia kwa kiasi kikubwa kuwapa fursa watendaji na viongozi kuzifahamu vyema taasisi zao.

“Kama Wizara ya Fedha hatofanya wajibu wake hakuna litakaloendeleo, kwani lolote tunalotaka kulifanya basi ni lazima lipate fedha na fedha hutafutwa”alisema Dk. Shein.

Aidha, alisema kuwa iwapo uwajibikaji utakwenda vizuri mafanikio zaidi yanapatikana na kuupongeza uongozi wa Wizara hiyo kwa kufanya wajibu wao na kusisitiza kuwa kila Wizara ikitekeleza vyema wajibu wake mapato yataongezeka.

Alieleza kuwa Serikali haiendeshwi na mtu mmoja bali kila mmoja hufanya kwa wajibu wake na kazi zake na kueleza juhudi zilizochukuliwa mara baada ya kuingia madarakani ambapo kabla ya hapo makusanyo ya Serikali kwa mwezi yalikuwa ni Bilioni 13.5 ambapo Uongozi huo ulieleza kuwa Mashirika yaliomo katika Wizara hiyo yamekuwa yakienda vizuri na kupata faida kwa kiasi kikubwa

hivi sasa makusanyo ni bilioni 60 kwa mwezi.

Alisema kuwa yote hayo ni utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM, na kueleza haja kwa kila mmoja kufanya kazi kwa nidhamu, bidii na maarifa.

Dk. Shein alitumia fursa hiyo kumpongeza kiongozi wa TRA Zanzibar kwa kufanya kazi vizuri, pamoja na Kamishna wa ZRB kwa kukusanya vyema mapato ya Serikali.

Alieleza haja ya kushirikikiana na sekta binafsi kwa kufanya kazi pamoja na kuwasaidia ili waweze kutekeleza shughuli nyengine muhimu za kimaendeleo ikiwa ni pamoja na kuimarisha huduma za kijamii na yale ya msingi  Serikali itayatekeleza.

Alieleza kuwa uchumi unaimarika kwa mashirikiano kati ya sekta ya umma na sekta binafsi.

Mshauri wa Rais wa Zanzibar Pemba Dk. Maua Abeid Daftari kwa upande wake alitoa pongezi kwa uongozi pamoja na watendaji wa Wizara hiyo na kusisitiza haja ya kuongeza kasi katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo zikiwemo barabara.

Uongozi huo pia, ulimpongezi Rais Dk. Shein kwa utaratibu mzuri alioweka wa mikutano hiyo inayoendelea ya kujadili mipangokazi ya Mawizara na kueleza kuwa Mashirika ya Wizara hiyo yanakwenda vizuri na kupata faida kwa kiasi kikubwa

Aidha, ulieleza kuwa kumekuwa na changamoto kubwa ya utoaji wa risiti na hivi sasa wapo katika hatua za mwisho za mfumo wa risiti ambapo matarajio ni mwishoni mwa mwaka huu ambapo wataanza kwa uhamasishaji.

VIJANA WAELIMISHWA JUU YA MADHARA YANAYOTOKANA NA MIMBA ZA UMRI MDOGO

Wazazi na walezi    wametakiwa kuwaelimisha vijana wao  juu ya madhara yanayotokana na mimba za umri mdogo ili  kujikinga na vitendo vitakavyosababisha kupata mimba katika umri huo.

Akizungumza katika mkutano  uliowashirikisha  waalimu wa madrasa , Masheha,  ngos  na wadau wengine huko katika skuli ya mohd juma pindua  Afisa kutoka shirika la UNESCO  kanda ya Zanzibar  Hasina  Salim amesema  iwapo jamii itashindwa  kukaa na watoto  wao  nakuwapatia  elimu hiyo  madhara ya mimba za utotoni  zitaendelea kuongezeka.

Kwa upande wake  mwalimu mkuu wa skuli ya secondari ya Mohd Juma Pindua  Ali Simai Makame  ameahidi kuifikisha elimu wqalioipata  kwa jamii  kupitia kwa wanafunzi  walionao maskulini ili kuona  afya ya uzazai  inatekelezwa ipasavyo .

Akiakhirisha mkutano huo  wa siku mbili naibu mkurugenzi  elimu msingi Haji Kombo Kali  ameawataka washiriki kuitumia   elimu waliopata kuifikisha  kwa jamii  ili kuwanusuru vijana  na majanga yanayoweza kutokea .

Wakichangia mkutano huo washiriki hao walikuwa na haya ya kusema .

 

error: Content is protected !!