Recent Posts by asha

BARAZA LA USIMAMIZI NA UTOAJI WA LESENI KUANDAA MFUMO BORA WA UTOAJI WA LESENI

Waziri  wa biashara  na  viwanda  Balozi Amina Salum  Ali  ameliagiza Baraza  la  usimamizi  na  utoaji wa  leseni  kuandaa mfumo bora  wa utoaji wa leseni  ili  kuwapunguzia  wafanyabiasha mzigo  wa   utitiri  wa  tozo  mbali  mbali.

Balozi amina  ametoa  agizo  hilo  wakati  akizindua  bodi  ya  taasisi  hiyo  yenye dhamana  ya  kusimamia  leseni , amesema  kumekuwa  na tozo  nyingi  zinazotolewa  na  taasisi mbali mbali jambo linalowaongezea  gharama  wafanyabiashara  na  wanachi  kwa  kupanda  kwa  bei.

Amewasisitiza  wajumbe  wa  bodi  hiyo  kukaa  pamoja  na  kuandaa mfumo  utakaofanya  leseni  kutolewa  katika  kituo  kimoja na  kuachana  na  utaratibu  uliopo  sasa  kwa baadhi ya taasisi kufanya majukumu yanayofanana katika sekta moja.

Mwenyekiti  wa  bodi  hiyo  nd,  Vuai  Mussa  ameahidi  kwa  wajumbe  wa  bodi  hiyo  kutekeleza  majukumu  waliokabidhiwa  kwa  umakini  na  uadilifu  pamoja na matatizo yaliyopo na  dhamira  na  malengo  ya  Serjkali  katika  kuimarisha  sekta   ya  biashara.

 

MKUTANO WA MAKATIBU WAKUU WA NCHI 16 WANACHAMA WA JUMUIYA YA MAENDELEO KUSINI MWA AFRIKA (SADC)

Katibu mkuu wizara ya afya, maendeleo ya jamii, jinsia, wazee na watoto nd Zainabu Abdi Chaula amefungua mkutano wa makatibu wakuu wa nchi 16 wanachama wa jumuiya ya maendeleo kusini mwa Afrika (SADC)ambao utajadili   agenda 13 ikiwemo kifua kikuu na ukimwi .

Akifungua mkuatano huo Bi Zainabu Chaula amesema mkutano huo umewashirikisha  makatibu wakuu kutoka nchi 16 za   SADC ambapo  utajadili masuala mbalimbali ya afya ambapo amebainisha kuwa malengo ya SADC kuwa ifikapo mwaka 2030 ugonjwa wa kifua kikuu uwe umeisha katika nchi za kusini mwa afrika .

Amezitaja agenda ambazo zitajadiliwa katika mkutano huo ambao  utaongozwa na sekretariet ya sadc ni pamoja na masuala ya ukimwi, maambukizi ya virusi vya ukimwi ,tb,chanjo,malaria masuala ya lishe kuimarisha mifumo ya afya, huduma za afya ya uzazi pamoja na kupunguza vifo kwa mama wajawazito.

Nae Mkurugenzi mtendaji wa tacaids dkt. Leonard Maboko amesema tanzania imefanya vizuri katika masuala ya tohara kwa wanaume ukilinganisha na nchi 16 za sadc.

Pia amesema mkutano huo  utajadili mambo ambayo yatasaidia kupunguza maambukizi mapya ya virusi vya ukimwi kwa kutoa elimu kwa makundi mbali mbali.

Kauli mbiu ya mkutano huo ni ushirikiano wa nchi za sadc ni nguzo kuu ya kufikia maelendeo endelevu ya sekta ya afya na mapambano dhidi ya ukimwi

MATUMIZI YA VITAMBULISHO VIPYA VYA MZANZIBARI KUHIFADHI KUMBUKUMBU ZA MATUKIO

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Ali Mohamed Shein amesema matumizi ya vitambulisho vipya vya Mzanzibari mkaazi Smart Card yataiwezesha serikali kuweka na kuhifadhi kumbukumbu za matukio ya watu wote katika daftari la usajili na utambuzi.

Dk. Shein amesema hayo katika uzinduzi wa Kadi mpya za Kielektronik ya Mzanzibari mkaazi, hafla iliyofanyika katika ukumbi wa Sheikh Idrisa Abdul wakil Kikwajuni mjini hapa.

Alisema matumizi ya vitambulisho hivyo vitaisaida Serikali, taasisi na watu binafsi kupanga vipaumbele vya utekelezaji wa shughuli mbali mbali zenye mnasaba na huduma za maendeleo ya kijamii.

Aidha, alisema kuwepo kwa mfumo huo wa matumizi ya vitambulisho vipya utaisadia serikali katika kuwatambuwa watu wanaostahiki kupata haki za msingi , kama ilivyobainishwa katika Katiba ya Zanzibar ya 1984.

“Itawezesha kumtambua mtu anaestahiki kupata haki yake kama vile malipo ya pensheni, haki za matibabu, kujiunga na masomo na nyenginezo”, alisema.

Dk. Shein alisema kutokana na vitambulisho hivyo Serikali itapata urahisi  katika suala zima la ukusanyaji wa mapato hivyo kuimarisha huduma muhimu za kijamii, ikiwemo afya, elimu, barabara pamoja na ulinzi na usalama wa raia na mali zao.

Alisema kimsingi Serikali inapaswa kuwa na nyenzo katika udhibiti wa amani na utulivu wa watu wake, hivyo ni dhahiri Vitambulisho vipya vitakavyotumika hivi sasa ni vyenye ubora wa hali ya juu na uwezo  wa kuhifadhi taarifa  nyingi za mtumiaji.

Alieleza kuwa vitambulisho hivyo vimetengenezwa kwa teknolojia ambayo sio rahisi kughushiwa, vikiwa na uwezo mkubwa wa kiusalama wa taarifa za mtumiaji, akibainisha kutumika  katika nchi kadhaa duniani.

Rais Dk. Shein alitowa wito kwa wakaazi wote wa Zanzibar waliofikia umri wa miaka 18 kwenda kujisajili katika ofisi za Wakala wa Usajili wa matukio ya Kijamii zilizopo katika Wilaya zote nchini, sambamba na wale ambao bado hawajajiandikisha kufanya hivyo.

Aidha, aliwataka watendaji wanaohusika na utayarishaji wa vitambulisho hivyo, kuwa makini na waangalifu katika utoaji wake.

Vile vile aliwataka Wakuu wa Mikoa kusimamia vizuri taarifa za uhakiki wa watu walioko katika maeneo yao, kuanzia ngazi za shehiya, wadi na Wilaya ili kuhakikisha wanawatambua wananchi wao na taarifa zao zilizo sahihi.

“Ni muhimu mlifanyie mapitio daftari la wakaazi katika shehiya, ambalo ndio msingi wa uthibitisho wa kujua taarifa za utambuzi na makazi ya watu waliomo katika maeneo yenu”, alisema.

Dk. Shein aliwataka wananchi kutambua jukumu la kuisadia Ofisi ya Wakala wa Usajili wa matukio ya kijamii katika kutambuwa wakaazi wa maeneo yao badala ya kuiachia jukumu hilo Ofisi hiyo pekee.

Aidha, aliwataka wananchi kuondokana na tabia ya kutumia njia za mkato katika upatikanaji wa vitambulisho hivyo, akibainisha hatua hiyo imekuwa chanzo cha kuibuwa rushwa.

“Naendelea kukunasihini watendaji wote wa Wakala wa Usajili wa matukio ya kijamii Zanzibar, mfanye kazi zenu kwa uadilifu, uzalendo na mfungamane na misingi ya haki na sheria pamoja na kufuata taaribu zilizowekwa katika kuendesha Ofisi ”, alisema.

Alisisitiza haja ya kulinda na kudumisha amani na utulivu uliopo nchini, akibainisha kuwa ni hazina isiyopaswa kuvurugwa na kusema bila ya kuwepo amani na utulivu nchini, hakutakuwa na meendeleo yoyote yatakayofikiwa,

Alisema kukamilika kwa mradi huo ni miongoni mwa hatua za utekelezaji wa Ilani ay Chama cha Mapinduzi ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2015-2020, inayolenga kuwapatia huduma bora wananchi.

Katika hatua nyengine, Dk. Shein aliwakumbusha wananchi umuhimu wa kutembea na Kadi ya Utambulisho wa Mzanaiabari mkaazi mahala popote ndani ya nchi, akibainisha faida kubwa ya jambo hilo.

Mapema, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa, Serikali za mitaa na Idara maalum za SMZ, Haji Omar Kheir aliwataka wananchi wote wenye sifa za kisheria kufika katika vituo vya usajili vilivyopo kila Wilaya nchini.

Alisema vitambulisho vipya vya Mzanzibar mkaazi ndicho kitakachotumika katika upatikanaji wa huduma mbali mbali muhimu kama vile upatikanaji wa leseni, miamala ya fedha, mahitaji katika taasisi za umma pamoja na zile zenye mahitaji ya vitambulisho.

Aidha, alisema Wizara hiyo itaendelea kusimamia utoaji wa elimu kwa wananchi ili kutii sheria ya ukaazi na kupata fursa mbali mbali ziliopo nchini.

Nae, Mkurugenzi Mtendaji wa Wakala wa Usajili na matukio ya kijamii Zanzibar, Dk. Hussein Khamis Shaaban alisema Ofisi hiyo itaendelea na mikakati ya kusajili na kuwapatia vitambulisho wananchi wote wenye sifa za kisheria.

Alisema mfumo wa vitambulisho  vya kielektronic ni ufunguo katika kufikia maendeleo ya kiuchumi, kijamii na kisiasa pamoja na kudumisha ulinzi na usalama katika nchi.

Aidha, alisema Zanzibar inakabiliwa na changamoto kubwa ya uingiaji wa wageni kutoka nje, hivyo kuwepo kwa vitambulisho hivyo ni muhimu kwani kutawezesha kuwatambuwa wageni hao.

Katika hafla hiyo, pamoja na mambo mengine, Dk. Shein alipata fursa ya kutembelea Ofisi za Wakala wa Usajili wa matukio ya Kijamii Zanzibar ziliopo Mazizini na kuangalia vifaa mbali mbali vinavyotumika kutayarishia vitambulisho hivyo.

Aidha,  Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa na Idara maalum za SMZ Haji Omar Kheri alimkabidhi Dk. Shein Kitambulisho kipya cha Mzanzibari mkaazi , ambapo nae alipata fursa ya kuwakabidhi  viongozi mbali mbali wa serikali , akiwemo Mama Mwanamwema Shein pamoja na Wananchi kadhaa.

 

 

 

KAMPUNI YA KIMATAIFA YA MILLICOM GROUP ITAENDELEA KUSHIRIKIANA NA ZANZIBAR

Makamu wa Rais wa Uhusiano wa Kampuni ya Kimataifa ya Millicom Group kutoka Miami Nchini Marekani Bibi Rachel Samren amesema taasisi hiyo itaendelea kushirikiana na Zanzibar  kuhakikisha huduma za Mawasiliano zinawafikia wananchi bila ya matatizo.

Amesema taasisi hiyo inayosimamia huduma za Mawasiliano ya Kampuni za Mitandao ya simu za mkononi za Zantel na Tigo imejipanga kuwapa huduma bora watumiaji wa mitandao hiyo.

Bibi Rachel Samren akiuongoza ujumbe wa viongozi wa Kampuni za Tigo na Zantel alisema hayo wakati akibadilishana mawazo na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi Vuga Mjini Zanzibar.

Alisema Millicom Group kwa sasa imefikia hatua nzuri ya kuungwa mkono kwake na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ushirikiano ambao hivi sasa umeshafikia asilimia 99.5%.

Bibi Rachel Samren alimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba kinachosubiriwa kwa sasa ni kukamilika kwa asilimia 5% iliyobakia inayohusiana na masuala ya kisheria.

Makamu wa Rais huyo wa Mahusiano wa Kampuni ya Kimataifa ya Millicom Group kutoka Miami nchini Marekani Bibi Rachel Samren aliishukuru na kuipongeza Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar chini ya watendaji wake waandamizi wa Serikali kwa hatua kubwa iliyofikiwa na mafanikio.

Naye kwa upande wake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi aliuhakikishia uongozi huo wa Kampuni ya Kimataifa ya Millicom Group kwamba Serikai ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kutoa kila aina ya msaada katika kuona azma hiyo inafanikiwa vyema.

Balozi Seif alisema Serikali kuu tayari imeshaazimia kukaribisha taasisi na Makampuni ya ndani na nje ya nchini katika kusaidiana na Serikali kwenye sekta za uwekezaji kwa lengo la kuimarisha Uchumi na kuongeza pato la taifa wakati maisha ya jamii yataendelea kustawi zaidi.

 

 

Recent Comments by asha

No comments by asha yet.

error: Content is protected !!