Recent Posts by TALHA FERUZ

SHIRIKA LA MAGAZETI YA SERIKALI KUPANUA WIGO WA SOKO WA KUSAMBAZA MAGAZETI ZANZIBAR

Uongozi wa Shirika la Magazeti ya Serikali umetakiwa kupanua wigo wa soko kwa kusambaza magazeti ya Zanzibar leo, The Spoti na ‘Zanzibar Mail’ katika maeneo mbali mbali ya mikoa ya Zanzibar ili yaweze kuwafikia kirahisi wananchi.

Hayo yameelezwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein wakati akipokea taarifa ya utekelezaji wa mpango kazi wa Wizara ya Habari, Utalii na Mambo ya Kale kwa kipindi cha kuanzia Julai hadi Disemba, 2019/2020.

Alisema  shirika hilo linaweza kupata mafanikio makubwa na kuongeza kiwango cha uchapishaji wa magazeti kutoka kopi 3,000 zinazochapishwa hivi sasa hadi kufikia kopi 5,000 kwa kuzisambaza katika vituo mbali mbali mikoani kwa kutumia  vipando vya kawaida  kama vile Bajaji.

Aidha, Dk. Shein amesisitiza umuhimu wa Wizara hiyo kusimamia, kuzienzi na kutunza nyaraka na kumbukumbu za serikali, kwa kuzingatia kuwa ndio uhai na utajiri wa Taifa.

Mapema, akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa mpango kazi wa Wizara hiyo, Waziri wa Habari, Utalii na Mambo ya Kale Mahamoud Thabit Kombo alisema katika kipindi hicho Wizara ilifanikiwa kutekeleza miradi mbali mbali katika idara na taasisi zake, ikiwemo uimarishaji wa maeneo ya Kihistoria ya Mvuleni, Mwinyimkuu na Mkamandume, (awamu ya pili) yaliotengewa jumla ya shilingi 300,000,000/.

Alisema katika eneo la kihistoria la Mvuleni,  kampuni ya KIN INVESTIMENT iinayoshughulikia ujenzi huo tayari imesafisha eneo lote la mradi pamoja na kujenga jengo jipya la kutolea huduma pamoja na vyoo vitakavyotumiwa na wageni watakaofika eneo hilo.

Aidha, alisema katika kipindi hicho Wizara ilipokea ujio wa ndege kadhaa, ikiwemo  kutoka nchi za Russia, Uganda na Poland ambazo zimekuwa zikifanya safari za moja kwa moja kutoka nchini mwao hadi Zanzibar.

Vile vile alisema Wizara kupitia Wakala wa Uchapaji wa serikali imeanza kujenga jengo la ghorofa mbili linalotarajiwa kuwekwa mitambo mipya na ya kisasa, ukiwemo mtambo wa kuchapisha madaftari ya wanafunzi wa Serikali.

Katibu mkuu kiongozi na katibu wa baraza la mapinduzi Dk.Abdulhamid Yahya Mzee, Mshauri wa Rais wa Zanzibar wa masuala ya Mambo ya Kale  Ali Mzee, Naibu wa Waziri wa Wizara Bi.Chum Kombo Khamis na viongozi mbali mbali kutoka katika Wizara,Idara mbali mbali pamoja na mashirika nao walipata nafasi ya kuzungumzia masuala mbali mbali yanayohusiana na wizara hio.

 

MWENGE WA UHURU KUJENGA HAMASA KATIKA KUSTAWISHA MAENDELEO YA KIJAMII

 

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Vijana, ajira na Watu wenye Ulemavu Mh. Jenista Muhagama amesema kufanyika kwa uzinduzi wa Mwenge wa Uhuru katika Mikoa mbali mbali ya Tanzania inawajengea uwezo Vijana kutambua historia ya Nchi katika harakati za kujipatia uhuru.

Akizungumza mara baada ya ziara ya kuangalia matayarisho ya maandalizi ya Uwanja unaotarajiwa kuzinduliwa mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka huu huko Makunduchi, amesema Serikali zote mbili ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania na ya Zanzibar inatambua mchango mkubwa wa vijana hivyo kushiriki kwao kunajenga hamasa katika kustawisha maendeleo ya kijamii chini ya misingi ya umoja Amani na Utulivu Nchini.

Nae Waziri wa Vijana, Utamaduni, sanaa na Michezo Balozi Ali Karume amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imethamini heshima iliyopewa ya kuzindua wa mbio hizo mwaka huu hivyo itahakikisha inashrikiana na uongozi wa Mkoa wa Kusini katika kufanikiwa maandalizi hayo.

Mkuu wa Wilaya ya kati Nd. Hamida Mussa Khamis na Mkuu wa Wilaya ya Kusini Nd. Idrissa Kitwana Mustafa wamesema shughuli za awali za maandalizi zinaendelea katika hatua ya kuridhisha na kuahidi kuyafanyia kazi maelekezo yote waliyopewa.

WILAYA YA KASKAZINI B IMESEMA ITAHAKIKISHA DAWA YA KUMALIZA MALARIA INAPIGWA KATIKA NYUMBA ZOTE

Uongozi wa Wilaya ya KaskaziniB imesema itahakikisha dawa ya kumaliza Malaria inapigwa katika Nyumba zote zilizokusudiwa katika Shehia za Wilaya hiyo.

Mwenyekiti ya Kamati ya Ulinzi na Usalama Nd. Rajaba Ali rajab ya Wilaya hiyo amesema uzoefu unaonesha kuwa kuna baadhi ya Wananchi wanakataa Nyumba zao kupigiwa dawa kwa sababu zisizokuwa na msingi  hali inayokwamisha mpango wa kumaliza Malaria kutofikiwa

Akizungumza katika mafunzo ya Wafanyakazi wa upigaji   dawa Majumbani unaotarajiwa kuanza Februari 15 Wilaya Kaskazini B amefahamisha kuwa watahakikisha kazi hiyo inafikiwa kwa kushirikiana na Kamati ya ulinzi na Usalama.

Rajab ambae pia ni Mkuu  wa Wilaya  hiyo amewataka Masheha kutoa taarifa haraka kwa Watu watakaokaidi kupigiwa dawa hiyo ili kuchukuliwa hatua kwa vile Serikali inatumia gharama kubwa kutokomeza ugonjwa huo Zanzibar.

Jumla ya Shehiya Nane za Wilaya hiyo ya Kaskazini B zinatarajiwa kupigwa dawa ya kuulia Mbu wa Malaria ikiwemo Kiwengwa, Mangapwani, Zngwezingwe,  Karange, Mahonda, Kiombamvua, Kidanzini, Upenja.

MH. SIMAI MOH’D SAID AMEZITAKA KAMATI ZA SKULI KUSHIRIKIANA NA VIONGOZI WA WIZARA

Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Nd. Simai Moh’d Said amezitaka Kamati za Skuli kushirikiana na Viongozi wa Wizara hiyo ili kuleta Maendeleo ya Elimu kwa Wanafunzi.

Ameyasema hayo katika Mkutano wa Makabidhiano ya Dakhalia ya Wanaume ya Skuli ya Sekondari ya Moh’d juma Pindua kati ya Balozi wa Japan Nchini Tanzania Nd. Simchi Gonto na Skuli ya Sekondari Moh’d Juma Pindua huko bBaraza la Mji Mkoani Pemba.

Nae Balozi wa Japani Nchini Tanzania Simchi Gonto amesema Japan itaendelea kutoa   misaada ya mahitaji maalum kupitia mfuko wake na kuona kuwa Vijana wanalijenga Taifa na kuwa kiungo muhimu kati ya Tanzania na Japani.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Kusini Pemba Nd.  Hemed Suileman Abdallah ametoa shukrani kwa Balozi wa Japan  kwa kuwapatia Dakhalia hilo kwani litawasaidia kuchochea ari ya Wanafunzi kuwa na hamasa ya kusoma na kuinua ufahamu katika masomo yao.

 

Recent Comments by TALHA FERUZ

No comments by TALHA FERUZ yet.

error: Content is protected !!