BALOZI SEIF AMEWATAKA WAWEKEZAJI WA TANZANIA NA UTURUKI KUSHIRIKIANA KATIKA MIRADI YA KIUCHUMI

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi amesema wawekezaji wa Tanzania na Uturuki wanapaswa kuutumia uhusiano uliopo wa pande hizo mbili kushirikiana katika kuwekeza Miradi ya Kiuchumi.

Balozi Seif Ali Iddi alitoa kauli hiyo Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar wakati alipofanya mazungumzo na ujumbe wa Viongozi Waandamizi wa Kampuni za Kimataifa za Gökyol na Dayk kutoka Nchini Uturuki waliofika Nchini Tanzania kuangalia maeneo wanayoweza kuwekeza katika nyanja ya miundombinu ya ujenzi.

Alisema Mataifa mengi ulimwenguni yamekuwa na uhusiano wa Kidiplomasia kwa miaka mingi baada ya uhuru ambapo kwa sasa uhusiano huo unastahiki kuelekezwa zaidi kwenye Diplomasia ya Kiuchumi itakayoweza kusaidia kustawisha maisha na maendeleo ya Wananchi walio wengi.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliushauri Uongozi wa Kampuni hiyo kutenga muda mahsusi utakaowapata wasaa mpana zaidi wa kuangalia maeneo yanayostahiki kuwekezwa na Kampuni yao iliyoanza kuonyesha  Azma ya kutaka kutumia fursa zilizopo Nchini Tanzania.

Alisema Zanzibar na Tanzania kwa ujumla zimekuwa na maeneo mengi yenya ushawishi wa kuimarishwa miundombinu yake hasa katika Sekta ya Ujenzi na Mawasiliano yenye kuchukuwa nafasi kubwa ya ukuzaji Uchumi wake kupitia bidhaa zinazotokana na Sekta ya Kilimo zinazostahiki kuingia katika Soko.

Naye Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji Zanzibar Nd. Mustafa Aboud Jumbe alisema zipo bara bara zisizopungua 11 katika maeneo mbali mbali ya visiwa vya unguja na pemba ambazo tayari zimeshafanyiwa uchambuzi yakinifu zikisubiri fedha kwa ajili ya ujenzi wake.

Nd. Mustafa aliueleza ujumbe huo wa Viongozi Waandamizi wa Kampuni ya Kimataifa ya Dayk kutoka Nchini Uturuki kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Wizara hiyo iko tayari kushirikiana na  wadau wa maendeleo katika kuona Bara Bara hizo zenye urefu wa kilomita 150 zinajengwa na kutoa huduma nzuri.

Kwa upande wa Sekta ya Usafiri wa Baharini, Nd. Mustafa alisema jitihada zinaendelea kuchukuliwa na serikali katika kutafuta mbinu za kuipanua Bandari kuu ya Malindi ili iwe na uwezo wa kutoa huduma kwa Meli kubwa za Mizigo zaidi ya moja kwa wakati mmoja.

Mapema Viongozi hao Waandamizi wa Kampuni za Kimataifa za Gökyol na Dayk kutoka Nchini Uturuki walisema Kampuni zao zilizoasisiwa tokea miaka ya 1961 na 1971 zina uzoefu wa kimataifa katika Ujenzi wa Miundombinu ya Bara Bara kuu {Highway} pamoja na majengo ya Hospitali na Skuli.

Walisema Wahandisi wa Kampuni hizo waliobobea  hutekeleza Majukumu yao yanayokwenda sambamba na kushiriki katika Shughuli za Kijamii katika maeneo na Nchi wanazopata fursa za kushiriki katika Miradi Mikubwa ya Kimataifa.

Comments are closed.

error: Content is protected !!