Blog

MWENGE WA UHURU KUJENGA HAMASA KATIKA KUSTAWISHA MAENDELEO YA KIJAMII

 

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Vijana, ajira na Watu wenye Ulemavu Mh. Jenista Muhagama amesema kufanyika kwa uzinduzi wa Mwenge wa Uhuru katika Mikoa mbali mbali ya Tanzania inawajengea uwezo Vijana kutambua historia ya Nchi katika harakati za kujipatia uhuru.

Akizungumza mara baada ya ziara ya kuangalia matayarisho ya maandalizi ya Uwanja unaotarajiwa kuzinduliwa mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka huu huko Makunduchi, amesema Serikali zote mbili ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania na ya Zanzibar inatambua mchango mkubwa wa vijana hivyo kushiriki kwao kunajenga hamasa katika kustawisha maendeleo ya kijamii chini ya misingi ya umoja Amani na Utulivu Nchini.

Nae Waziri wa Vijana, Utamaduni, sanaa na Michezo Balozi Ali Karume amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imethamini heshima iliyopewa ya kuzindua wa mbio hizo mwaka huu hivyo itahakikisha inashrikiana na uongozi wa Mkoa wa Kusini katika kufanikiwa maandalizi hayo.

Mkuu wa Wilaya ya kati Nd. Hamida Mussa Khamis na Mkuu wa Wilaya ya Kusini Nd. Idrissa Kitwana Mustafa wamesema shughuli za awali za maandalizi zinaendelea katika hatua ya kuridhisha na kuahidi kuyafanyia kazi maelekezo yote waliyopewa.

DK.SHEIN AMEITAKA WIZARA YA ELIMU ZANZIBAR KUREJESHA MICHEZO MASHULENI

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein ameitaka Wizara ya Elimu na Mafunzo ya amali kujidhatiti na kuwa na programu maalum ya mafunzo itakayowezesha kuwa na walimu wa kutosha wa masomo ya Sayansi, ili kuondokana na upungufu uliopo kwa walimu wa kada hiyo.

Dk. Shein amesema hayo Ikulu Jijini Zanzibar, wakati akipokea taarifa ya utekelezaji ya mpango kazi wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali kwa kipindi cha kuanzia Julai hadi Disemba, 2019.

Alisema ni vyema Wizara ikaandaa utaratibu wa muda mfupi utakaowawezesha wahitimu wa Sekondari waliofaulu vyema masomo ya Sayansi  pamoja na wale wanaomaliza shahada katika vyuo vikuu nchini, kujiunga katika mafunzo hayo na hatimae kugaiwa katika skuli mbali mbali.

Alisema katika kipindi cha miaka 56 tangu Mapinduzi ya 1964, sio jambo jema kwa Zanzibar kubaki na tatizo la upungufu wa walimu wa Sayansi na kuendelea kutegemea misaada ya walimu kutoka nje ya nchi.

Alieleza kuwa Wizara hiyo ni ya kitaaluma na yenye watendaji weledi na wenye uzoefu, hivyo ni vyema wakajipanga ili kumaliza  kabisa kadhia hiyo iliodumu kipindi mrefu.

Aidha, alishauri Wizara hiyo kuandaa na kutuma waraka maalum Serikalini juu ya azma ya kuwa na maktaba mpya ya kisasa itakayojikita katika matumizi ya mitandao.

Alisema kupitia sekta tofauti Zanzibar imekuwa ikianzisha majengo mbali mbali ya kisasa, hivyo ni muhimu pia kuwa na maktaba ya kisasa ili kuchochea maendeleo ya kielimu nchini.

Vile vile,  aliishauri Wizara hiyo kutuma mapendekezo  Serikalini  kuangalia uwezekano wa kuwaajiri walimu  800 wanaofundisha katika vituo vya Tutu Unguja na Pemba, kwa kuzingatia uzito wa kazi hiyo yenye kuweka misingi bora ya kitaaluma kwa wanafunzi.

Rais Dk. Shein, alitaka Wizara hiyo kuangalia uwezekano wa kuwa na skuli mbili zaidi za Wanawake mikoani, kutoka miongoni mwa skuli tatu zinazoendelea kujengwa, ili kufanya jumla ya skuli za jinsia hiyo kufikia nne Unguja na Pemba.

Vile vile, alibainisha umuhimu wa kuwepo utaratibu maalum wa kuwafikia wananchi wasiojua kusoma na kuandika katika shehiya mbali mbali nchini, ikiwa ni hatua ya kuondokana kabisa na jamii isiyojuwa kusoma na kuandika.

Akigusia umuhimu wa kufanya tafiti kwa mustakbali mwema wa maendeleo ya elimu nchini, Dk. Shein aliutaka uongozi wa Wizara hiyo kukaa na kufikiria namna ya kuwa na taasisi ya ‘elimu na utafiti’  na vipi itakavyofanya kazi.

Alipongeza hatua ya uongozi wa Wizara hiyo ya kufanya ukaguzi wa mara kwa mara katika skuli, kwa kigezo kuwa huchangia mabadiliko chanya, hivyo akataka juhudi hizo kuendelezwa kwa kuzingatia sheria, sera, kanuni  na miongozo ya Wizara bila ya kuathiri imani za kidini.

“Ukaguzi ni jambo zuri sana, ubora wa elimu unakuja kutokana na ukaguzi”, alisema.

Katika hatua nyengine, Dk. Shein aliutaka uongozi wa Wizara hiyo kurejesha vuguvugu la michezo skulini  katika ngazi za msingi na Sekondari kama ilivyokuwa miaka iliyopita.

Alisema Serikali ilianzisha Idara ya michezo, ambapo pamoja na mambo mengine lengo lake ni kuchochea vuguvugu la michezo mbali mbali katika skuli Unguja na Pemba, hatua iliyoliletea sifa kubwa taifa.

Alisema katika miaka iliyopita kila skuli ilikuwa na walimu na vipindi maalum vya michezo na hivyo kuibuwa ushindani katika michezo tofauti, jambo alilobainisha hivi sasa limepotea.

Alisisitiza umuhimu wa kufufua ushindani wa kimichezo katika skuli, ukiwemo ule wa ‘Inter House competition’ kwa kuanzia.

Aidha, aliutaka uongozi wa Wizara hiyo kufanya juhudi kubadili mitazamo na fikra ghasi za baadhi ya wazee kuwa michezo inaviza ufahamu na maendeleo ya wanafunzi , jambo alilobainisha sio sahihi kwa kigezo kuwa  ‘elimu na michezo’ ni mambo yenye uwiano na yanayokwenda sambamba.

Nae; Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi Dk. Abdulhamid Yahya Mzee, aliupongeza uongozi na watendaji wa Wizara hiyo kwa maandalizi bora ya taarifa iliotumwa, sambamba na utekelezaji mzuri wa majukumu yao.

Mapema, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Riziki Pembe Juma, alisema katika kipindi hicho Wizara hiyo imepata mafanikio makubwa katika utekelezaji wa mpango wa elimu wa mwaka 2019/2020, hatua iliyokwenda  sambamba na utekelezaji wa Ilani ya CCM ya 2015-2020.

Alisema mafanikio hayo yamechangiwa na upatikanaji mzuri wa fedha, ambapo hadi kufikia Disemba, 2019 Wizara ilifanikiwa kupata jumla ya shilingi 100,838,538/ (sawa na asilimia 82) ya makisio ya nusu mwaka.

Alisema miongoni mwa mafanikio hayo ni pamoja na kuongezeka kwa ufaulu wa wanafunzi katika mitihani ya kidato cha nne 2019 katika daraja la kwanza, pili na la tatu.

Alisema katika kipindi hicho idadi ya watahiniwa waliofaulu daraja la kwanza walikuwa 299, ikilinganishwa na watahiniwa 185 waliofaulu katika mitihani ya 2018.

Aidha, alisema katika uimarishaji wa miundombinu, skuli tisa kati ya skuli 12 za ghorofa zinazojengwa zimekamilika na kufunguliwa katika shamrashamra za maadhimisho ya miaka 56 ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Alieleza kuwa Wizara tayari imezipatia  samani na vifaa vya maabara skuli zilizofunguliwa pamoja na vitabu vya masomo mbali mbali, vikiwemo vya maktaba za skuli.

Waziri Pembe aliyataja mafanikio mengine yaliopatikana katika kipindi hicho kuwa ni muendelezo wa ujenzi wa vituo 22 vya Ubunifu wa Sayansi Unguja na Pemba,   vinavyotarajiwa kukamilika katika  mwaka huu wa bajeti.

“ Tumefanikiwa kuimarisha huduma za Dakhalia zote za Unguja na Pemba kwa kuzipatia usafiri dakhalia mbili kati yake na kusaidia gharama za chakula kwa wanafunzi wote wanaokaa dakhalia”, alisema.

Aidha,  alieleza  jumla ya seti 11,560 za vikalio vya wanafunzi watatu watatu wa madarasa ya msingi vilinunuliwa kutoka nchini China, ambapo hatua za kuvisafirisha zikiwa zinaendelea, huku awamu ya kwanza ya seti 2015 za vikalio hivyo kwa ajili ya wanafunzi 6,045 vikiwa tayari vimewasili katika Bandari ya Zanzibar.

Vile vile alisema katika kipindi hicho Skuli za Sekondari za Serikali zimeingiziwa fedha katika akaunti za skuli zao, jumla ya shilingi 2,114,608,500/ kwa ajili ya kufuta michango ya wazazi katika elimu.

Katika hatua nyengine,  Waziri huyo alisema katika utekelezaji wa mpango huo changamoto mbali mbali zilijitokeza, ikiwemo uhaba wa vitabu vya elimu ya sekondari kwa wanafunzi wa kidato cha kwanza na cha Pili, hususan kwa masomo ya Fizikia, Kemia na Baiolojia.

Alisema  pia kulikuwa na changamoto katika uimarishaji wa miundombinu ya madarasa kwa ajili ya kupunguza msongamano wa wanafunzi na kufikia kigezo cha wanafunzi 45 kwa darasa ngazi ya msingi na wanafunzi 40 kwa sekondari, na kubainisha kuwa  hivi sasa  wastani wa wanafunzi 81 husoma darasa moja katika ngazi ya elimu ya msingi na wanafunzi 62 ngazi ya sekondari.

Alisema tatizo jengine ni kuwepo uhaba wa wataalamu wa maabara, maktaba na ICT katika skuli pamoja na uhaba wa vifaa vya kufundishia somo la TEHAMA.

DK.SHEIN AMESISITIZA HAJA YA WIZARA YA VIJANA KUSHIRIKIANA KATIKA KUTEKELEZA MAJUKUM YAO

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amesisitiza haja kwa Wizara ya Vijana, Utamaduni, Sanaa na Michezo kushirikiana kwa pamoja ili kutekeleza majukumu yao hasa ikizingatiwa kwamba Wizara hiyo inagusa sekta muhimu katika jamii.

 Hayo aliyasema leo, Ikulu Jijini Zanzibar alipokutana na uongozi wa Wizara ya Vijana, Utamaduni, Sanaa na Michezo wakati ilipowasilisha utekelezaji wa Mpango Kazi  kwa kipindi cha Julai hadi Disemba 2019/2020.

Rais Dk. Shein alitumia fursa hiyo kumpongeza Waziri wa Wizara hiyo pamoja na viongozi wengine na wafanyakazi wote kwa mashirikiano waliyonayo katika kuiendeleza Wizara hiyo.

Aliipongeza taarifa iliyowasilishwa na Wizara hiyo na kusisitiza haja ya kushirikiana katika Idara zote za Wizara hiyo kwani Wizara ni yao wote isipokuwa wanatofautiana kwa kazi wanazozifanya.

Rais Dk. Shein alieleza haja kwa Wizara hiyo kukaa pamoja na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali kwa lengo la kusaka vipaji vya michezo mbali mbali hapa Zanzibar.

Rais Dk. Shein alieleza kuwa hatua hiyo itasaidia kwa kiasi kikubwa katika kushirikiana katika kuibua vipaji kwenye michezo kadhaa ambayo hivi sasa imeanza kupoteza sifa kutokana na kukosa wachezaji ukiwemo mchezo wa mpira wa pete.

Katika maelezo yake Rais Dk. Shein alisisitiza haja kwa uongozi wa Wizara hiyo kuyatunza na kuyaendeleza mambo ya utamaduni wa Mzanzibari hasa kwa zile tamaduni ambazo zinatoweka hivi sasa zikiwemo ngoma, vyakula na vivazi vya asili.

Rais Dk. Shein alisisitiza haja ya vijana kuwezeshwa kwa kupewa fedha na nyenzo ili waweze kuendeleza miradi yao mbali mbali huku akieleza juhudi zinazochukuliwa na Serikali za kuwawezesha vijana huku akieleza azma ya kuundwa kwa Wizara hiyo.

Sambamba na hayo, Rais Dk. Shein alieleza haja ya viongozi hao pamoja na wafanyakazi wa Wizara hiyo kuwa wazalendo na kupenda vya kwao sambamba na kufanya kazi kwa mapenzi na uadilifu.

Alieleza kuwa Zanzibar iko karibu sana na viongozi wa Chama cha mpira duniani FIFA na viongozi wa CAF pamoja na vyama vyengine vyote vya michezo duniani hiyo ni kuonesha kuwa Zanzibar inapendwa na inathaminiwa.

Nae Katibu Mkuu Kiongozi na Katibu wa Baraza la Mapinduzi Dk. Abdulhamid Yahya Mzee aliipongeza kazi nzuri ya uwasilishaji iliyofanywa na Wizara hiyo na kueleza haja ya vijana kuandaliwa mipango madhubuti itakayowasaidia katika maisha yao.

Mapema Waziri wa Wizara hiyo Balozi Ali Abeid Karume alieleza kuwa Wizara hiyo imefanikiwa kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015-2020 kwa kiasi kikubwa hasa katika sekta ya michezo.

Kwa upande wa vijana alieleza kuwa, vijana wamewezeshwa katika shughuli za kiuchumi kwa kupatiwa vifaa mbali mbali vya kujiendeleza pamoja na kupatiwa nafasi za mafunzo kazi ili kuweza kujiajiri wenyewe kwa lengo la kuinua pato lao na la Taifa.

Kwa upande wa utamaduni, Balozi Karume alisema kuwa Wizara imeendelea kuazimisha matamasha mbali mbali likiwemo tamasha la utamaduni wa Mzanzibari, kukiendeleza kikundi cha Taifa cha taarab kwa kukipatia vifaa na ofisi.

Akieleza kuhusu lugha ya Kiswahili alisema kuwa kongamano la Kimataifa la lugha hiyo limekuwa likifanyika kwa kushirikisha wataalamu na magwiji wa lugha hiyo kutoka ndani na nje ya nchi na kueleza jinsi Wizara hiyo inavyokuza michezo ya asili ukiwemo mchezo wa ng’ombe.

Aidha, Wizara hiyo ilimpongeza Rais Dk. Shein kwa azma yake ya kuanzisha Studio ya Filamu na Muziki iliyopo Rahaleo ambapo wasanii, Taasisi za Serikali pamoja na watu binafsi wamekuwa wakiitumia kwa shughuli mbali mbali za Sanaa na kijamii.

Aliongeza kuwa Wizara hiyo imefanikiwa kuzindua program ya Ajira kwa Vijana kwa awamu ya kwanza ambapo jumla ya vijana 3,300 (Unguja 2,102 na Pemba 1,198) wamenufaika na programu hiyo.

Mapema Katibu Mkuu wa Wizara ya Vijana, Utamaduni, Sanaa na Michezo Omar Hassan (King), alitumia fursa hiyo kueleza utekelezaji wa Malengo kwa robo mbili kuanzia mwezi wa Julai hadi Disemba 2019/2020.

 

WADAU WA SEKTA YA UTALII WAMETAKIWA KUWEKA WAZI HATUA ZA KUTATUA KASORO ZA UENDESHAJI WA SEKTA HIYO

Waziri wa Habari Utalii na Mambo ya Kale Mh.Mahmoud Thabit Kombo amewataka Wadau wa Sekta ya Utalii kuweka wazi hatua za kutatua kasoro za uendeshaji wa Sekta hiyo Zanzibar zilizochukuliwa kwa pamoja na Serikali .

Akizungumza katika Kikao kati ya Wadau wa Sekta ya Utalii na Viongozi wa Jumuiya ya kuratibu masualaya Utalii ya Nchini Italia, amesema hatua hiyo itawezesha kupunguza malalamiko kutoka kwa Wawekazaji  wa Sekta hiyo inachangia pato kubwa la Taifa.

Waziri Mahmoud amefahamisha kuwa miongoni mwa juhudi hizo  ni pamoja kuimarisha huduma na ujenzi wa Uwanja wa Ndege, na  Barabara mbalimbali na pamoja na kuanzishwa mfumo wa Kisasa wa kupata  Viza  kwa Wageni kwa njia ya Kielektroniki.

Viongozi wa Jumuiya hiyo ya kuratibu masuala ya Utalii ya Nchini Italia, wamesema wamesisitiza kuwekwa Mfumo bora wa ulipaji Kodi kulingana na misimu ya Wageni wanavyotembele Nchini.

Jumuiya hiyo inayotambulika kwa jina la Astoi Confindustria Viaggi inaratibu Safari za kiasi ya  Watalii  laki moja na nusu wanaotembelea Zanzibar  kwa Mwaka.

error: Content is protected !!